KUHUSU SISI
KUHUSU
SISI
KITABU MARKET ni moja ya bidhaa za JAMVI
LA SIMULIZI. Hii ni maktaba, ni duka la vitabu ni uwanja wa maarifa. Ni mahali
ambapo utazunguka rafu na mashubaka ya vitabu usiyamalize. Lakini JAMVI LA
SIMULIZI ni kitu gani?
JAMVI
LA SIMULIZI ni jukwaa la fasihi andishi lililosheheni simulizi mbalimbali.
Jukwaa hili lilianzishwa mwaka 2012 ikiwa ni moja ya ndoto za Richard Mwambe, ambaye
ndiye muasisi. Lilianza katika mitandao ya kijamii hususan Facebook na
Wahatsapp. Na kupitia jukwaa hilo wapenzi wa fasihi waliweza kusoma riwaya za
kusisimua na zenye taharuki katika mfululizo wa visa vya kusisimua vya Kamanda
Amata.
Lakini pia, simulizi kutoka kwa
waandishi rafiki zilisomwa pia. Jamvi la simulizi limekuwa jukwaa la
kuwatangaza waandishi wengine na kuzitangaza kazi zao.
RICHARD MWAMBE
Muasisi wa JAMVI LA SIMULIZI amezaliwa miongo minne iliyopita, mtoto wa sita katika familia ya watoto nane waliozaliwa na Mwl. Richard Amour na Bernadetha Lukanga. Amekulia katika viunga vya Ukonga jijini Dar es salaam. Amelelewa na mikono yenye upendo zaidi ya ile minne iliyozoeleka. Ni mtu wa watu, mwenye upendo na kupendwa.
Elimu ya msingi ameipata katika Shule ya Msingi Ukonga 1988-1994, kisha akaendelea kupambana na maisha mengine hasa katika masuala ya kiufundi.
Uandishi wake wa riwaya unachangizwa na marehemu baba yake aliyemuhamasisha kusoma vitabu katika umri mdogo na kumtaka siku moja kuandika vya kwake.
Mkono wake umeandika litania ndefu ya simulizi za kusisimua za kijasusi na kipelelezi mbali ya mapenzi na maisha.
Yeye ni Fundi mbobevu wa Umeme wa majumba na viwanda pamoja na umeme jua, Mjuvi kiasi kwenye mifumo ya Kompyuta mwenye cheti cha CISCO. Pia ni msanii wa sanaa za jukwaani na muandishi wa riwaya, miswada ya filamu na mtambaji hadithi. Elimu hii ya uandishi na sanaa ameipata katika Taasisi ya Sanaa Bagamoyo.
Pamoja na yote hayo pia ni muasisi na Mkurugenzi wa NGO ya KITABU MAISHA yenye ofisi yake Mjini Iringa.