MKATABA WA KIFO (Jiue Mwenyewe)

By: richard MWAMBE

0
Available Stock:

MKATABA WA KIFO (Jiue Mwenyewe)

UTANGULIZI

Saa moja usiku huo, vijana wa TSA wakiwa full package walikuwa hewani na chopa la kijeshi ambalo daima hulitumia kwa kazi zao, wakielekea huko. Scoba kama kawaida yake, alikuwa akiliongoza chuma hilo. Walihakikisha wanapita upande ambao watu wanaowataka wasishtuke. Daima Chiba alikuwa akiwaangalia kupitia kompyuta yake katika mfumo wa satellite.

“Tafuta sehemu ya kutua, tumeshawaacha nyuma!” Chiba akamwambia Scoba. Hesabu zao hazikuwa haba. Tayari walikuwa juu ya Mto Ruaha. Scoba akatafuta eneo zuri ambalo kwalo angeweza kushusha ile chopa. Akalipata. Katika uwanja mdogo wa kijiji cha Igagala, wakatua. Dakika tatu zilizofuata tayari walikuwa nje wakiwasubiri, bunduki nzito zilikuwa vifuani mwa Kamanda Amata na Chiba na Gina huku wakiwa wamevalia mavazi ya kijeshi. Siku mojamoja walipenda kuvaa namna hii.

Kutoka kwenye moja ya kona zilizo pembezoni mwa milima hiyo ya Tao la Mashariki, mwanga wa taa za magari yaliyokuwa yakija ili kupita eneo hilo ulionekana. Baada ya kupita lori la mafuta na mizigo. Amata na Chiba waliingia barabarani na kusimama katikati. Naam, Landrover Count, mbili, nyeusi ziliibuka.

“Haohao!” Chiba akawaambia wenzake. Wakaziweka bunduki zao tayari. Scoba akasogea na kuwasimamisha. Yale magari yakatii amri na kusimama. Scoba akaliendea lile la mbele na kugonga kioo huku akitoa ishara ya kufunguliwa kioo hicho. Kikashushwa.

“Washa taa za ndani!” akawaamuru. Yule dereva akatii. Ndani ya lile gari mulikuwa na watu watatu, Wazungu; wawili wanaume na mmoja mwanamke. Scoba akawaangalia vizuri. Akawahoji maswali kadhaa kasha akawataka kushuka kufungua sehemu ya nyuma ya magari hayo.

“Mnataka nini?” Mzungu aliyekuwa akiendesha akauliza.

“Ukaguzi! Tunataka kukagua magari yenu! Shuka haraka!” Scoba akamwambia na yule jamaa akashuka akifuatiwa na wenzake. Katika gari la nyuma, kulikuwa na wengine wawili. Magari yale yote mawili upande wa nyuma yalifungwa barabara. Mtu wa nje hasingeweza kuona vilivyomo ndani.

“Sawa!” yule jamaa akajibu na kuzunguka nyuma ya lile gari huku Scoba akimfuata nyuma na bunduki yake ikiwa tayari kwa lolote. Amata na Chiba nao walifuata upande huu na ule. Katika gari la pili, hakuna aliyeshuka, lakini tayari waliona hali ya pale haina amani.

“Fungua!” Scoba akamwamuru yule jamaa naye akafungua ule mlango. “Weka mikono juu! Mtie pingu!” Scoba akamwambia Chiba. Scoba aliamuru baada ya kuona shehena ya bunduki hatari zilizopangwa kwenye rafu za chuma. Yule jamaa akatiwa pingu, na waliobaki nao wakashushwa na kutiwa pingu. Kutoka gari la pili wakajiandaa kwa mashambulizi. Mmoja wa wale waliokuwamo humo akaandaa bastola, tayari. Akampatia mwenzake na kumweka tayari. Wakati Scoba, Chiba na Amata wakishughulika na wale watu waliowakamata hawa jamaa wawili waliobaki kwenye gari jingine walitoka ghafla ili kuanzisha mashambulizi. Aliyekuwa nyuma ya usukani alipokanyaga ardhi tu, hata kabla hajakanyaga vizuri ardhi, yule jamaa alijikuta akitupwa upande mwingine na kuanguka kama mzigo. Roho yake ikauacha mwili. Risasi iliyopigwa kutoka mafichoni kwenya vichaka ilimaliza kazi iliyotumwa. Yule mtu wa pili alipoona mwenzake damu zikimruka akajua tayari, kumekucha, alicofanikiwa ni kufyatua risasi moja ambayo badala ya kumpata mlengwa ambaye ni Scoba, ikadidimia shingoni mwa mwenzake aliyekuwa na pingu mikononi. Kiwewe!

“Nooooo!” akapiga kelele na kujitoa kwenye ule mlango huku akifyatua risasi ovyo. Kabla hajaleta madhara, alijikuta akipaishwa juu na kubwagwa ukingoni mwa gema kubwa linaloelekea mto Ruaha. Gina alijitokeza lutoka kwenye moja ya kichaka akipiga mluzi.

“Hongera mwanamke!” Amata akamwampongeza.

“Asante!”

Nusu saa baadae gari la polisi likawasili mahali pale. Askari kutoka Mikumi, wakawasili wakiwa wametimia kwa zana. Wakatakiwa kufanya wanaloweza yale magari mawili yafikishwe kituoni kabla hayajarudishwa Dar es salaam. Zile maiti mbili na wale wengine wakapakiwa kwenye lile chopa na safari ya Dar es salaam ikaanza. 

Endelea kusoma riwaya hii bure kabisa...

View or Download Book
📘 View PDF ⬇ Download

Related Products

Product Image
ISABELA - Mpango Hasi

By: Richard R. Mwambe

Product Image
KITANZI CHA MWISHO

By: Richard Mwambe

Product Image
KIJASHO CHEMBAMBA - EP 01

By: Richard Mwambe

Product Image
PASIPOTI YA GAIDI - Kitabu Cha 1

By: Richard Mwambe