By: Richard Mwambe
Hujuma Na
Uzandiki
Mwandishi: Richard MWAMBE
SURA YA I
IKULU –
DAR ES SALAAM
Saa
10:30 alfajiri
|
W |
AKATI giza
likijiandaa kutoweka na kuipisha nuru ya asubuhi, miti yote ilikuwa imetulia
kana kwamba kuna aliyeiambia ifanye hivyo. Ni Tausi mmoja mmoja aliyekuwa
akilia alfajiri hii tena kwa nyakati tofauti. Hawakuwa na zamu ya kufanya hivyo
isipokuwa ilitokea tu, ndivyo walivyoumbwa. Hawakuwa wakijua lolote linaloendelea katika
maisha ya mwanadamu wakati huo, zaidi walisubiri kukuche waendelee kupendezesha
mandhari ya eneo hilo. Hawa walikuwa kivutio kikubwa sana katika eneo hilo kwa
wapiti njia.
Hekaheka katika jengo hilo la Makao Makuu ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ilikuwa kubwa. Vijana wa jeshi la polisi, kikosi maalum
cha kutuliza ghasia, walikuwepo wakiwa kimejiweka tayari kwa lolote, ijapokuwa
huwa hapo kwa lindo kila siku lakini leo hii walikuwa kivingine kabisa. Mbali
na wao, eneo hilo, afajiri hiyo lilizungukwa pia na vijana wa Jeshi la Wananchi
waliovalia kombati zao za mabakamabaka, wakiwa na silaha nzitonzito mikononi
mwao, kila mmoja akionekana kutingwa na shughuli inayompasa kufanya kwa muda
huo. Magari ya wagonjwa kutoka Jeshi la Wananchi yalikuwa yikifanya kazi ya
kubeba majeruhi na maiti zilizokutwa ndani ya jengo hilo, hekaheka.
Katibu Mkuu kiongozi akasimama katikati ya ukumbi mkubwa ndani
ya jengo hilo, alikuwa kimya bila kusema lolote. Macho yake yalijawa na
machozi, midomo yake ilibaaki ikimwemwesa.
“Samahani Mzee!” sauti ilisikika kutoka nyuma yake, alishtuka
kama mtu aliyekutana ghafla na mtoa roho,
akageuka na kumtazama kijana aliyemwita. Mzee huyo alijikuta anashindwa hata
kuitikia ile salamu au kuuliza anamwitia nini, badala yake alimfuata yule
kijana pindi alipoondoka eneo lile. Moja kwa moja walifika kwenye ukumbi mdogo
ambao ulikuwa na watu wasiozidi sita, yaani wale wenye vyeo vya juu, wenye
dhamana ya ulinzi na usalama wa nchi, pamoja nao kulikuwa na wasaidizi wengine
ambao ni maofisa wachache wa Ikulu. Akaketi katika kiti kilichokuwa wazi,
akiwatazama watu hawa kwa zamu, pamoja nao alikuwapo mtu mwenye cheo cha pili
kutoka kile cha mkuu wa nchi.
“Kama mnavyoona… maofisa kadhaa na wafanyakazi wa Ikulu
wameuawa,” Makamu wa Rais aliliambia jopo, “kilichotokea hapa hakieleweki,
hakuna anayejua nini kimetokea, ila mke wa Rais yaani First Lady ametoweka, nafikiri, kwa uwazi kabisa kuwa huu ni
uvamizi lakini sijui ni nani au siwezi kuhusisha na kikundi gani kwani uchunguzi
ndio kwanza umeanza,” akatulia kimya bila kusema lolote. Macho yake yalionekana
wazi kutona kwa machozi ambayo hayakutaka kumwagika.
“Bila shaka, inawezekana walidhamiria kumteka au kumdhuru Rais
mwenyewe, walipoona hayupo basi wameondoka na mkewe, First Lady. Kumbukeni, Ikulu ya Tanzania ni kati ya majengo
machache duniani yanayolindwa kwa mitambo ya hali ya juu na wanausalama
waliokomaa kwenye fani yao, lakini kama tumevamiwa, bila shaka, waliyovamia ni
kundi lenye weledi wa juu zaidi katika medani hii ya usalama,” waziri wa ulinzi
aliongezea na wajumbe wote wakatikisa vichwa.
“Tumepoteza vijana wetu makini kabisa ambao waliaminiwa sana na
mkuu. Taarifa nimeshamfikishia, na amekatisha ziara yake, anarudi nyumbani
kwani hali hii si ya kuvumilika, tunategemea neno la mwisho kutoka kwake,”
Makamu akalieleza baraza na wote wakaunga mkono.
“Mheshimiwa Makamu, naomba utoe tamko la wazi kwa sasa juu ya
hali hii, maana, tusipoangalia, waandishi wa magazeti kama kawaida yao wataanza
kutoa habari zisizothibitishwa,” msemaji wa Ikulu alimwambia Makamu wa Rais.
“Ok, naomba ieleweke hivi, Ikulu imevamiwa na kundi la kigaidi,
walinzi kadhaa wameuawa na bado kuna hali ya sintofahamu. Vyombo vya usalama
viko katika harakati za kuhakikisha vinategua kitendawili hiki ndani ya saa
chache. Tunaomba wananchi kuwa watulivu na pia kutoa taarifa polisi pindi
unapoona mtu unayemhofia katika maeneo yenu,” makamu wa Rais akazungumza. Punde
tu taarifa ile ikachapwa katika mashine na kusainiwa akakabidhiwa huyo bwana,
Msemaji wa Ikulu ili kuwafikishia wanahabari waliofika alfajiri hiyo katika
ukumbi mdogo wa maelezo ulio ndani ya jengo hilo.
✠
Ikulu ilikuwa haiingiliki mpaka uwe na kibali maalumu, vijana wa
Jeshi la Wananchi waliegesha magari yao upande wa baharini na mengine mawili
upande wa hospitali ya Ocean Road na nyingine zilisimama karibu na Ofisi ya
Hazina. Barabara ya Magogoni ilifungwa haikuruhusiwa gari wala mtembea kwa
miguu kupita eneo lile. Juu angani helkopta ya jeshi na polisi zilikuwa
zikifanya doria zikishirikiana na zile za Jeshi la Wananchi.
Kwa ujumla jiji la Dar es salaam lilikuwa katika misukosuko ya
hapa na pale. Majira ya saa sita mchana barabara kubwa na ya muhimu zaidi
katika jiji hilo ilifungwa kwa muda, ile inayotoka uwanja wa ndege kuelekea
mjini. Ving’ora vikasikika na gari kama saba hivi zilipita kwa kasi ya ajabu
kuelekea mjini. Na dakika kumi na mbili tua gari hizo ziliingia katika lango
kuu la Ikulu na kuegeshwa mahala pake wakati tayari Mkuu wa nchi alikuwa
amekwishashuka na kuingia ndani ya jengo hilo, moja kwa moja akiwa na walinzi
wake alipitiliza na kuteremka ngazi iliyompeleka katika chumba maalum ambacho
hufanyia mikutano yake ya siri kilichopewa jina la ‘Kilimanjaro Square’.
“Nimesikitishwa na kilichotokea, hii haiwezekaniki kuivumilia,
ni uvamizi,” Rais aling’aka huku akizunguka chumba badala ya kuketi chini. Watu
watano waliokuwa naye ndani ya chumba hicho walibaki kimya kabisa. Mkuu wa nchi
akarudi na kuketi mezani kwake, akakamata kalamu yake na kutaka kuandika kitu
lakini mkono ulikuwa mzito.
“Tulikuwa tunakusubiri wewe Mheshimiwa Rais ili utoe neno lako
vijana waingie kazini mara moja,” Makamu wa Rais alitamka.
“Oh! Shiiit, Come on, hii ni Cold War! Let me say Cold
War, na ntaipigana mpaka mwisho. Mtu kukuvamia ndani ya chumba chako na kumchukua
mkeo ni matusi, matusi yasiyovumilika!” akang’aka huku akisimama wima kwa
hasira, “Ni jengo gani au taasisi gani Afrika ina ulinzi mkali na makini kama
hili jengo hapa? Hakuna, ninyi mnajua na dunia inajua. Sasa hawa waliokuja na
kufanikiwa kufanya madhara haya ina maana wamejuaje njia za kuingia humu na
njia za kutokea kama si hujuma?” aliendelea kung’aka kwa sauti. Kisha akatulia
kidogo huku kijasho kikimtiririka, mwili wake ulimtetemeka kama mtu asikiaye
baridi kali. Akasimama na kutazamana na Mkuu wa Majeshi “Nataka vijana wako
waliobobea kweye michezo hii wahakikishe wanampata First Lady ndani
ya saas12.
“Umesomeka Amiri Jeshi Mkuu,” akajibu mkuu wa majeshi na
kusimama akatoa saluti ya utii.
“Na ninyi wengine muwe katika kazi zenu za kawaida lakini nyote
muangaze macho katika sakata hilo,” akatoa maagizo kwa viongozi wa vikosi
vingine. Nao wakaitikia wito huo na kila mmoja akaondoka katika jengo hilo
lililotukuka. Ni dakika hiyohiyo tu ambapo ule ukumbi ulikuwa na watu wawili tu
yaani Rais na Makamu wake.
“Inaniuma sana Mheshimiwa!” Rais alimwambia makamu wake huku
mikono yake ikiwa haitulii sehemu moja.
“Mimi pia, ukizingatia tumepoteza vijana wenye ujuzi wa hali ya
juu sana katika maswala ya usalama,” makamu naye alijibu.
“Nina uhakika kwa vijana wetu hawa wa JW, hao wahalifu
watapatikana tu,” Rais akajibu.
“Sawasawa kabisa, lakini unafikiri wao peke yao wataweza
kulibaini kundi hilo lililofanya kadhia hii?”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Kwa sababu kutokana taaluma yao nahisi kama kazi hii inaweza
kuwa ngumu,” makamu alikazia.
“Hapana! Hata mimi nilikuwa mwanajeshi, najua, tuna idara ya
upelelezi ya jeshi, na kutokana na uzito wa jambo hili, wao ndio watu muafaka.”
Akameza mate kisha akaendelea, “Unajua hawa lazima wapambane na mtu
anayelingana nao kwa sababu bila shaka ni magaidi sasa gaidi ni levo nyingine,
lazima apambane na mtu wa levo yake na hao si wengine ni vijana wa jeshi,”
Mheshimiwa Rais alamwelekeza makamu wake juu ya mpango huo. Kikao cha wawili
hao kilipomalizika, Makamu wa Rais akaondoka na kumwacha mkuu wake peke yake
ndani ya ofisi hiyo. Kitendo tu cha Makamu wa Rais kutoka na kumwacha
mheshimiwa peke yake, simu ya mezani ilianza kuita kwa nguvu na fujo.
Mheshimiwa Rais akaingalia kwa tuo kabla hajaamua kama ainyanyue na kuisikiliza
au aiache, lakini tatizo ni kwamba hakujua simu hiyo ilikuwa inahusu nini au
inamhusu nani. Na mara nyingi simu ya chumba hicho ikiita basi huwa kunakuwa na
jambo zito la kiofisi. Kwa mkono wa kitetemeshi aliukwanyua mkono wa simu ile
na kuiweka sikioni bila kuongea lolote.
“Usijaribu kuchukua hatua yoyote kwa kumtafuta mkeo, tunajua unampenda na ndiyo maana tumemchukua, lakini ujue sisi tunachokitaka si fedha wala hatuna ugomvi na wewe. Tunahitaji jambo moja tu, toa amri ya kuondoa majeshi yako ya kulinda amani katika Kusini mwa nchi ya Ngoko. Ukilitekeleza hilo, mkeo utampata, na husipotekeleza tutateka na watu wa familia yako waliobakia, na wewe utakuwa wa mwisho…”....
NB: Riwaya hii ina mfululizo wa vitabu vinne; 1. Hujuma na Uzandiki, 2. Double Agent, 3. Anguko la Kizito na 4. Kazi Nzito
Ukitaka vitabu vinaavyofuata, tafadhali ingia kwenye huduma ya malipo kwa kuchagua category ya NUNUA KITABU
By: richard MWAMBE
By: Richard R. Mwambe
By: Richard Mwambe
By: Richard Mwambe