K.OK.W.A - 08

By: Richard Mwambe

0
Available Stock:

Ilipoishia.....

“Tuliambiwa tumuue Selina, huyu tuliambiwa ni mwanamke hatari sana hapa Tanzania…” akaeleza. Amata akashtuka kusikia hivyo. Selina ni Madam S. “Pia tulitakiwa kumuua Kamanda Amata!” akaendelea kusema. Amata alihisi kuingiwa na ubaridi kuanzia utosini mpaka unyayoni.

“Enhe!” akamtaka kuendelea.

“Pia tulitakiwa kumuua Geophrey Kisinini na Tabia Ismail,” yule bwana akaeleza pasi na kumumunya maneno. Kamanda Amata akajikuta anaishiwa nguvu. Akameza mate na kuitazama saa yake. Ilikuwa ikiyoyoma kuelekea saa tisa usiku. “Maiko mlikutana naye wapi hapa Dar es salaam?” akauliza.

“Tulikutana naye nyumbani kwake Kibada…” akajibu.

“Kibada? Ok! Nikikwambia unipeleke unaweza?” Amata akauliza. Yule bwana akajibu kwa kutikisa kichwa kwamba ‘ndiyo’. Wakati akihojiana na bwana huyo, tayari daktari alikuwa amewasili na kazi ya kushona masikio ya Braison ilianza. Amata akatoka kwenye kile chumba na kurudi katika ofisi ile ya upelelezi Mkoa. Pale akamkuta Inspekta Simbeye peke yake.

“We mshenzi siyo binadamu hata kidogo…” Simbeye akasema.

“Tukiwa kazini hatuna mzaha hata kidogo. Asante mzee mi nimemaliza, sasa huyo ni wa kwenu siyo wangu tena. Mimi niachieni yule mwingine bado sijamalizana naye,” Amata akamwambia, “tuonane kesho, nitalutafuta,” akamwambia huku akipotelea nje. Kamanda Amata akamchukua askari wa mapokezi na kumkabidhi vifaa vyote vya Braison Sambala kisha yeye akaingia garini. Gina alikuwa amelala fofofo nyuma ya usukani.

“We msichana, amka twende…” akamwambia Gina huku akimtikisa. Gina akakurupuka na kujiweka vizuri. Akajifikicha macho.

“Uuuuh nimechoka sana… tunaelekea wapi, saa tisa sasa…” Gina akauliza.

“Twende nyumbani kwako sasa tukalale…” Amata akamjibu. Gina akatabasamu na kuwasha gari.

“Hayo ndiyo maneno dear… nimemiss sana joto lako…”

“Endesha gari!”

 

✠ ✠

 

            Nyumbani kwa Gina, Msasani nyuma ya Supermarket ya Mayfair Plaza waliwasili saa tisa usiku. Wakati Gina akioga na kujiandaa kupanda kitandani, mwili ukiwa chem-chem, Amata alikuwa mezani katika chumba cha kujisomea. Juu ya meza hiyo palikuwa na simu na kitabu kidogo cha kumbukumbu. Vilikuwa vitu alivyovitoa kwenye chumba cha Braison Sambala. Akiwa ametingwa na simu yake, alihisi kuguswa bega.

            “Mpenzi muda wa kulala sasa, twende tafadhali,” sauti ya Gina iliyapenya masikio yake huku mkono wake mmoja ukiwa umepita nyuma ya shingo ya Amata na vidole vya mkono huo vikipapasa kifua cha mwanaume huyo. Amata alitaka kujibu, lakini alijikuta pumzi inamkatika. Mwanamke huyu alizijua batano zote za Amata; wapi ya kushusha na kupandisha sauti, wapi ya kupandisha na kushusha mapigo ya moyo na kadhalika. Hakuongea kitu, akainuka na kuambatana na mwanamke huyo mpaka chumbani. Haikuwachukua hata dakika kumi, wawili hao waligalagazana kitandani huku ndimi zao zikipishana kwa ufundi mkubwa kutoka kinywa cha huyu kwenda kinywa cha mwingine. Dakika arobaini na tano zilizofuata, kiu kilikuwa kimekatika. Gina alijitupa aliuchapa uzingizi mzito kifuani pa Amata. Lakini mwanaume huyo bado akili yake haikuwa sawa. Alikuwa akiwaza mengi kiasi kichwani mwake. Alitaka kujua jambo kabla jimbi hajawaika ili ajue akitoka humo ndani ni wapi pa kuanzia. Kokwa! Kokwa ilishaanza kumchanganya. Kichwani mwake tayari alianza kumhitaji Chiba. Kuna mambo huyu jamaa inabidi kuja kuyatatua! Akawaza. Akiwa katika mawazo hayo akajikuta akibebwa na usingizi mzito hasioutegemea.

            Sauti ya jimbi wa alfajiri ndiyo ilimgutusha kutoka katika usingizi huo. Alipojipapasa kifuani, hapakuwa na Gina, alipogeuza macho kuangalia pembeni, hakumuona mwanamke huyo. Amata akakurupuka na kuketi kitandani. Taa ya chumbani ilikuwa ikiwaka, mlango ulirudishiwa kama kawaida. Ni Gina tu hakuwamo mle chumbani. Akainuka na kusimama wima sakafuni. Akavuta hatua kuuelekea mlango wa kile chumba na kuufungua taratibu.


Burudika kupitia PDF

View or Download Book
📘 View PDF ⬇ Download

Related Products

Product Image
Dira Ya Maendeleo 2050

By: Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania

Product Image
PASIPOTI YA GAIDI - Kitabu Cha 1

By: Richard Mwambe

Product Image
MKATABA WA KIFO (Jiue Mwenyewe)

By: richard MWAMBE

Product Image
KITANZI CHA MWISHO

By: Richard Mwambe